Ni siku chache zimepita tangu msichana mmoja, mwanafunzi
wa kike katika chuo kimoja huko kanda ya ziwa anipigie simu akiomba ushauri
ikiwa kama anaweza kufanya biashara ya duka la nguo rejareja akiwa bado anaendelea
na masomo yake chuoni.
Katika kazi hii ya uandishi mara nyingi nimekukutana na maswali hasa ya vijana wanafunzi wa vyuo wenye nia na shauku ya kutaka
kuanzisha biashara wangali bado wanasoma na jambo moja lililonistaajabisha
sana ni kugundua karibu wanafunzi hao wote wana tabia moja inayofanana
utafikiri huambiana kabla ya kuuliza maswali yao, nitakwenda kuielezea tabia
hiyo ya ajabu hivi punde tu endelea kusoma.....
Mwanafunzi huyo wa kike wa chuo sitaweza kumtaja kwa
majina yake halisi wala utambulisho wake mwingine wowote ule kwani hajanipa
ruksa na badala yake hapa nitamuita tu kwa jina bandia la Katarina.
Katarina alitaka kujua ni mbinu na mikakati ipi ambayo
anaweza kuitumia ili biashara hiyo ya nguo iweze kuendelea na kushamiri pasipo
yeye kuwa pale muda wote wala kuathiri muda wake wa masomo chuoni.
Na mimi kama nilivyokwishawahi siku za nyuma kutoa majibu
kwa vijana wengine mbalimbali hapa, nilimwambia hilo ni jambo linalowezekana
kabisa lakini ni sharti ahakikishe anampata msaidizi mwaminifu atakayekuwa
akifanya kazi ya mauzo dukani.
Kwa kuwa duka la kuuza nguo rejareja ndio lilikuwa wazo
lake la kwanza, niliendelea kumsisitizia pia umuhimu wa matumizi ya mbinu na
mifumo ya uthibiti wa mapato ya duka la rejareja iliyoelezwa katika kitabu cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJATOLEO LA 2025 & GENGE na kabla hata sijamaliza Katarina akaniambia, “Nataka hicho kitabu ili niweze kujifunza
hiyo mifumo nikiwa nimetulia na kuchagua nitumie upi kwenye biashara yangu ya
nguo”
Hakusita akalipia shilingi elfu 10 chapchap
kama uonavyo muamala aliotuma hapo juu baada ya kukosea namba kidogo nikatuma
upya, na mimi nikamtumia kitabu chake. Zilipita kama siku mbili hivi akiwa
anakisoma na kisha nikaona tena namba ya simu yake ikiita.
Hapa sasa ndipo utapata lile jibu la swali nililoahidi
nitalijibu baadae, kwamba ni tabia gani ya kushangaza wanafunzi wote wa chuo
wanaotaka kuanzisha biashara wangali bado chuoni wanayo pasipo hata wao wenyewe
kujua kama wanayo.
Karibu wanafunzi wote wa vyuo wanaonipigia simu ama
kutuma ujumbe mfupi wakitaka niwashauri juu ya kuanzisha biashara wangali bado
chuoni wakisoma wana tabia moja inayofanana, huwa hawaulizi swali moja na
kuishia hapo.
Watarudi tena na tena kuuliza kiasi kwamba ikiwa wewe ni
mtu usiyependa usumbufu unaweza kuwablock au kuonyesha kukereka.
Lakini binafsi yangu mimi tabia yao hii hainikeri bali
inazidi kunitia hamasa zaidi na ari ya kuwasaidia ninapokumbuka namimi pia kuna
nyakati nilikuwa napitia kipindi kama chakwao na jinsi nilivyokuwa natamani kudadisi
masuala ya biashara au ubunifu mwingine wowote ule wa kuleta maendeleo. Naona
fahari kuwaonyesha njia sahihi ili siku moja wafanikiwe maishani.
Nakumbuka kuna mwanafunzi mmoja aliyekuwa akifuatilia
masomo yangu kwa email kipindi fulani akiwa anasoma sekondari, akawa ananipigia
simu kutaka ushauri kwangu. Aliendelea kunisumbua na maswali hata pale
alipoingia chuo kikuu akiniambia bado hana uiwezo wa kulipia vitabu au course
zangu za uandishi wa michanganuo.
Hata hivyo na mimi sikukata tamaa wala kuacha kumtumia masomo
kwa email. Kijana yule alipokuja kuhitimu Chuo kikuu alikuja kugeuka kuwa mteja
wangu mkubwa akinunua karibu vitabu vyangu vyote na semina, na mpaka sasa hivi
ninapoandika hapa ni muajiriwa mahali fulani lakini kando akimiliki miradi
kadhaa ya kiuchumi inayomuingizia kipato kizuri cha ziada.
Tukirudi tena kwa Katarina aliponipigia simu kwa mara ya
pili, safari hii alitaka nimshauri jambo jingine. Katika mawazo ya biashara
alizokuwa amefikiria kuanzisha mbali na biashara ya duka la kuuza nguo rejareja,
alikuwa na wazo jingine mbadala ikitokea la nguo akaliacha, la kuanzisha
biashara ya miamala ya simu, kutoa na kuweka pesa kupitia Tigo pesa au Mix by
Yas, M-pesa, Airtel Money, Azam Pesa nk.
Sasa akataka kufahamu ikiwa pia mifumo iliyoelezwa kwenye
kitabu ingeweza ikatumika na huko pia. Kimsingi nilimjibu ndiyo inawezekana
ijapokuwa biashara ya miamala ni tofauti kidogo kwani hushughuliki na stoku ya
bidhaa bali fedha taslimu na kwa kadiri fedha zilivyokuwa nyeti basi inahitaji
usimamizi wa kipekee zaidi hasa kwa yule utakayemwachia biashara mfano
kutokumwachia akae na fedha taslimu mkononi kwa muda mrefu zaidi ya siku moja kuepuka vishawishi vya kudokoa.
Katika makala yangu nyingine moja ya ushauri kwa mwanafunzi anayetaka kuanzisha biashara akiwa bado anasoma isemayo;-Biashara & uwekezaji mwanafuzi anaweza kuanza akiwa chuo, kidato cha 5, 1, darasa la 1 hata chekechea kuna mahali nilitoa ushauri huu ufuatao;-
“Kama ni lazima
mwanafunzi ufanye biashara, basi wekeza katika miradi isiyohitaji sana muda na
uwepo wako pale lakini pia epukana na miradi yenye hatari kubwa”
Mwishoni Katarina alikata shauri ya kubaki kwenye
biashara ya nguo shauri ya hatarai nyingi tulizoziona kwenye biashara ya
miamala ya simu kwa mazingira yake binafsi na siyo kama haiwezekani kabisa
hapana.
Katarina hakuishia hapo alikuja kunipigia tena simu mara ya tatu na safari hii aliniambia ya kuwa alikuwa amewasiliana na jamaa yake
mwingine wa karibu ambaye naye anamiliki biashara ya duka la kuuza nguo
rejareja jijini Mwanza.
Huyu jamaa yeye licha ya kumtajia mpaka eneo zuri la
kuanzisha hii biashara, alimshauri pia biashara akaifungue Mwanza mjini kuliko
na mzunguko mkubwa wa watu badala ya eneo la awalii alilokuwa amepanga ambalo
ni kijijini (Wilayani) japo pamechangamka kidogo na panafanyika minada ya vitu
mara 2 kwa wiki.
Nilimuuliza maswali machache mojawapo likiwa ni ikiwa
huyo mshauri mwingine ana maslahi yeyote binafsi anayoweza kuwa anayalenga
kutoka kwake pengine ya kifedha kiuhsiano wa mapenzi au hata ikiwa ni dalali.
Lakini majibu yake yalinidhihiririshia pasi na shaka kuwa ‘mentor’ huyo hakuwa na maslahi yeyote mengine yaliyojificha zaidi
tu ya kutaka msichana huyu aweze kutimiza dhamira/malengo yake ya kumiliki
biashara ya nguo akiwa bado anasoma
Basi ndipo na mimi nilipoungana na yule mshauri namba 2
na kumwambia Katarina kuwa ikiwa upo uwezekano wa biashara hiyo kuanzishwa
mjini, hakuna sababu ya msingi akaifungulie kijijini licha ya wasiwasi wake
mkubwa kwamba eti kodi ya pango la fremu ya biashara mjini ilikuwa ni shilingi
milioni mbili kwa mwaka kiasi ambacho ni kikubwa mno. Nikamtia moyo kwamba kodi
ya pango kubwa lakini pakiwa na mzunguko
mkubwa wa biashara siyo ishu (tatizo)
Nilimsihi kitu cha kwanza afanye utafiti wa soko mahali
hapo huyu mshauri alipomwelekeza kujiridhisha ikiwa kama kweli pana wateja na
biashara itaweza kutoka vizuri, achunguze na biashara za wengine kama yakwake
(washindani wake watarajiwa) mauzo yao yanaweza kufika shilingi ngapi kwa siku
nk.
Kulingana na lengo lake la kuwa na biashara inayozunguka
chapchap ili iweze kumudu gharama za kumlipa mfanyakazi huku na yeye akipata
faida nilimwambia aachane na wazo la kwenda kufungua biashara hii kijijini kwa
madai ya gharama kuwa kidogo kwani itamchelewesha.
Midhali mtaji aliniambia anao wa kutosha kulipia kodi ya
fremu hata ya miezi sita na kiasi kingine kubaki kwa ajili ya kununulia bidhaa
za nguo, usajili wa TIN namba na leseni ya biashara, nilimwambia maneno
yafuatayo,
“Jitoe
mhanga kachukue hiyo fremu ufanye biashara, huwezi kufanikiwa pasipo ‘kutake
risk’ ila hakikisha hakuna mazingira yeyote yale ya utapeli yanayoweza kuwepo
baina yako na yule mshauri uliyeniambia amekutafutia eneo la kufanyia biashara”
Nilimwambia Katarina pia kwamba mbinu na mifumo
aliyojifunza kwenye kile kitabu cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA
2025 & GENGE NDANI YAKE hususani ule mfumo wa kudhibiti
mapato yasiibiwe hata shilingi na msaidizi utafanya kazi kwa ufanisi zaidi
endapo tu “turn over” ya biashara
ni kubwa nikimaanisha kwamba mzigo unaisha chapchap na kwenda kununua mwingine
haraka jambo linalosababisha faida kuongezeka upesi (good ROI) na kufanya gharama zilizotumika kuanzisha biashara kurudi
kwa kipindi kifupi sana kijacho kabla hata hajamaliza chuo (short break even point)
Habari hii kuhusiana na safari ya Msichana Mwanafunzi wa
chuo Kikuu anayetaka kumiliki biashara angali bado chuoni akisoma haijaishia
hapa kwani ndio kwanza anafanya utafiti kusudi aje aanze.
Nakuahidi nitakupa mrejesho (Updates) kadiri mambo yatakavyokuwa yakiendelea na hata ikibidi uje
ufahamu ikiwa kama alifanikiwa ama la, kwani kwa jinsi nijuavyo mimi tabia za
wanafunzi wa chuo, Katarina hataishia pale aliponiuliza mara ya pili na ya tatu,
atarudi tena na tena kuniuliza mambo mengine mengi na mimi nimejiandaa kumpatia
majibu ya kina yatakayomsaidia kwenye safari yake hii muhimu kabisa maishani ya
kumiliki uchumi wake mwenyewe.
Makala hii imeandaliwa na
Peter Augustino Tarimo
Whatsap/Call: 0765553030
SOMA NA HIZI HAPA PIA;
1.
Kuanzisha biashara nikiwa chuoni nasoma nipeni ushauri nina
wakati mgumu
2.
Ushauri kwa mwanafunzi aliyehitimu chuo/masomo anayetaka kuanza
3.
Biashara nzuri 4 mwanachuo anaweza kufanya na mtaji wa
laki 2 huku akisoma
4.
Msomi chuo kikuu, UDSM amiliki biashara yake
5.
Biashara ya laini na miamala ya simu kwa mwanafunzi wa chuo
kikuu, mtaji laki 3 –ushauri
7. Biashara ndogondogo zenye faida ya haraka tanzania ni hizi
hapa, zipo nne(4)
9. Biashara 7 nzuri za kufanya zitakazokuingizia pesa hata kama umelala
10. Somo:mamilionea vijana 10 wakisimulia siri za utajiri wao
walivyofanikiwa
0 Response to "ENEO LA BIASHARA YA DUKA LA NGUO REJAREJA, JE NIFUNGUE MJINI AU KIJIJINI?-MWANAFUNZI WA KIKE CHUO KIKUU"
Post a Comment